Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limepokea gari aina Toyota Land Cruiser kutoka benki ya CRDB ambalo litasaidia kuongeza kasi na ufanisi katika kupambana na matukio ya uhalifu.
Kamanda wa Kanda hiyo, Lazaro Mambosasa amesema gari hilo litaongeza ufanisi wa kazi za jeshi la polisi ambapo litatumika kupambana na matukio ya uhalifu kwa kuyafikia maeneo mengi kwa haraka.
“Huu msaada ni uwezeshaji ambao utanijengea uwezo ili kutimiza majukumu yangu ya kazi bila kukwama hivyo gari hili litatumika kufanya doria na kupambana na matukio ya uhalifu na nitahakikisha jiji la Dar es Salaam linakuwa salama ,”amesema Mambosasa.
Mambosasa amesema kutokana na ufinyu wa bajeti kwenye Wizara ya Mambo ya Ndani hivyo ameziomba taasisi na wadau mbalimbali wajitokeze kulisaidia jeshi la polisi liweze kufanya kazi kwa ufanisi.
Pia amesema serikali imeshaanza kuhamia Dodoma hivyo jiji hili litabaki kuwa la kibiashara na linapokea wageni kutoka sehemu mbalimbali ndani na nje ya nchi.
Mambosasa amesema kutokana na jiji hilo kuwa la kibiashara hivyo wameimarisha ulinzi na usalama kwa wafanyabiashara ili kuhakikisha maendeleo yanakuwepo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Dk Charles Kimei amesema biashara haiwezi kukua eneo ambalo halina usalama hivyo wametoa gari hilo kwenda kwenye matukio kwa urahisi.
“Tumefurahi sana usalama wetu umerudi hivyo tumeona tutoe zawadi la gari ambalo litasaidia katika kupambana na uhalifu. Pia tunategemea kutoa gari lingine Machi mwaka 2018,”amesema Dk Kimei.
Post a Comment