Mtanange wa kirafiki kati ya timu ya taifa ya Benin na ile ya Tanzania ‘Taifa Stars’ utakaopigwa kesho Jumapili ndani ya Uwanja wa l'Amitie mjini Cotonou unatarajiwa kurushwa LIVE kupitia Azam TV.
Taifa Stars ambayo ipo chini ya kocha mzawa Salum Mayanga, akisaidiwa na Fulgence Novatus, Amy Ninje na Patrick Mwangata wameshawasili Cotonou na wameshaanza maandalizi ya mchezo huo ulio kwenye kalenda ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA).
Mkurugenzi wa Michezo wa AzamTV, Patrick Kahemele amesema kwamba mchezo huo utaonyeshwa na chaneli ya Azam Sports 2 kuanzia Saa 12:00 jioni kwa saa za Tanzania.
Kikosi cha Taifa Stars kilichowasili Cotonou kwa ajili ya mchezo huo, kinaundwa na makipa; Aishi Manula wa Simba SC, Peter Manyika wa Singida United na Ramadhani Kabwili wa Yanga SC.
Mabeki ni Boniphace Maganga wa Mbao FC, Abdi Banda wa Baroka FC ya Afrika Kusini, Gardiel Michael, Kevin Yondan wa Yanga, Nurdin Chona wa Tanzania Prisons na Dickson Job wa Mtibwa Sugar.
Viungo ni Himid Mao wa Azam FC, Mudathir Yahya wa Singida United, Hamisi Abdallah wa Sony Sugar ya Kenya, Jonas Mkude, Shiza Kichuya wa Simba, Ibrahim Hajib, Raphael Daudi wa Yanga, Simon Msuva wa Difaa Hassan El Jadida wa Morocco, Mohammed Issa wa Mtibwa Sugar, Farid Mussa wa Tenerife B ya Hispania na Abdul Mohammed wa Tusker ya Kenya.
Washambuliaji ni Mbaraka Yussuf wa Azam FC, Elias Maguri na Yohanna Nkomola ambao wote hawana timu kwa sasa.
Nahodha Mbwana Samatta alienguliwa kikosini mapema wiki hii baada ya kuumia akiichezea klabu yake, KRC Genk katika Ligi ya Ubelgiji na atakuwa nje kwa miezi miwili.
Post a Comment